TIMU YA WATAALAMU WA BONDE LA RUFIJI NYUMBANI KWA MZEE MAKOSA
Imewekwa: 04 Nov, 2024
TIMU YA WATAALAMU WA BONDE LA RUFIJI NYUMBANI KWA MZEE MAKOSA

Siku kadhaa tangu Waziri wa maji Mh.Jumaa Aweso atoe agizo kwa Bodi ya maji Bonde la Rufiji kufanya utafiti wa Maji kwaajili ya kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa Mzee Ramadhani Mrisho maarufu Makosa mkazi wa Mkoa wa Iringa ya kumchimbia kisima ili kiweze kumsaidia kutimiza adhima yake ya kuwa na Vitaru vya Miti itakayosaidia kutunza mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Agizo hilo tayari limetekelezwa ambapo wataalam wa Bodi ya maji Bonde la Rufiji wamefika nyumbani kwa Makosa ili kuifanya kazi hiyo ambayo imekamilika na kusubiri hatua inayofuata.

Akizungumzia utekelezaji wa Agizo hilo mbele ya wanahabari wa mkoa wa iringa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Fredy Haule amesema hatua zimechukuliwa ili kutimiza adhima ya Wizara kupitia Waziri wa Maji Jumaa Aweso ya kumsaidia Mzee Makosa ili kupata kisima cha maji kitakachomsaidia katika kumwagilia bustani za miche ya miti,anasema hiyo ni hatua kubwa yenye mafanikio kwani tija ya kazi hiyo itachangia kuhifadhi mazingira na kulinda hali ya kijani kupitia miti hivyo kazi inayofanywa na wataalamu wa bonde ikikamilika inafungua ukurasa kwa wakala wa Maji na Usafi wa mazingira Vijiiini RUWASA ambao ndiyo waliopewa jukumu la kuchimba kisima hicho.

"Ni kweli sisi kama Bonde tulipewa maelekezo na waziri wa maji tufanye utafiti kwenye eneo la Mzee Makosa ili achimbiwe kisima,tumepokea maelekezo hayo kwa uzito mkubwa na tayari wataalamu wetu wamefika kwenye eneo husika wanafanya kazi hiyo ili kupata majibu iwepo eneo hilo lina maji na baada ya hapo tutatoa taarifa kwaajili ya hatua zinazofuata"alisema Haule

Akiwa katika eneo hilo la utafiti Mtaalamu wa utafiti wa maji yaliyochini ya Ardhi kutoka bodi ya maji Bonde la Rufiji John Saimora anesema zoezi hilo linalenga kutafiti juu ya uwepo wa maji hivyo wao kama wataalamu wanaowajibu wa kuhakikisha wanatoa majibu iwapo eneo hilo linamaji au lah,

"Tumefika hapa leo ili tufanye utafiti kama ilivyo katika maelekezo ya waziri wa Maji Mh.Jumaa Aweso kwa lengo kumsaidia Mzee makosa ambaye anahitaji kisima kwaajili ya shughuli za uhifadhi,tunaimani kubwa kuwa zoezi hili litafanikiwa kwa kupata maji halafu shughuli zingine ziendelee"alisema