Miradi inayoendelea

1. Kuhamasisha Suluhisho Shirikishi za Kiasili Zinazoongozwa na Jamii kwa Ajili ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Usangu (Mradi P502536)

Mradi unalenga kuhamasisha suluhisho za kiasili za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Bonde la Usangu – Wilaya ya Mbarali. Mradi huu utasaidia kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya watu pamoja na mifumo ya ikolojia. Ili kusaidia jamii kukabiliana na mazingira yasiyotabirika, mradi utatambua na kuendeleza mbinu bora za usimamizi wa ardhi na maji (teknolojia za kilimo-ikolojia) zitakazoongeza kipato cha kaya, kukuza uzalishaji wa kilimo, na kuhakikisha ustawi endelevu wa mazingira.

Mradi huu unafadhiliwa kwa ruzuku kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wa Japan (JSDF) kupitia Benki ya Dunia (WB), na utatekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB) kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Juni 2025 hadi Novemba 2027.

Ili kuzingatia Viwango vya Kimazingira na Kijamii vya Benki ya Dunia (ESS), Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB) imeandaa Mpango wa Utekelezaji wa Masuala ya Mazingira na Jamii (ESCP), Mpango wa Ushirikishwaji wa Wadau (SEP) pamoja na nyaraka nyingine muhimu za mradi zitakazotoa mwongozo wa masuala ya mazingira na jamii wakati wa utekelezaji wa mradi. Wadau na pande nyingine zenye maslahi wanaweza kupata nyaraka hizi kupitia tovuti yetu.