Ndugu waandishi wa Habari,
Kama mnavyofahamu kila mwaka tarehe 5 Juni nchi yetu inaungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani. Maadhimisho haya hufanyika kutokana na maamuzi yaliyofanywa na shirika la umoja wa mataifa duniani mwaka 1972, linaloshughulikia mazingira duniani, kuwa kila tarehe 5 Juni kila mwaka itakua ni siku ya mazingira.
Kimataifa maadhimisho haya yatafanyika Pakistani yakiwa na kauli mbiu isemayo, “Ecosysteam Restoration” kwa Kiswahili ni “Kuongoa mfumo Ikolojia”. Na kwa kitaifa maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, ”Tutumie nishati mbadala, kuongoa mfumo Ikolojia” Kauli mbiu hii inahamasisha jamii kutumia nishati mbadala ili kuokoa vyanzo vya maji, misitu na uoto wa asili inayoendelea kuharibiwa kwani matumizi makubwa ya nishati ya mkaa yanapelekea kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na vyanzo vya maji na hivyo husababisha kuwepo na upungufu wa mtiririko wa maji katika vyanzo vya maji na kutopatikana kwa maji safi na salama.
Hivyo, katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, imekusudia kuungana na Watanzania wote katika kusaidia kuongoa mfumo ikolojia kwa kupanda miti katika vyanzo vya maji ili kurudisha wingi wa maji katika vyanzo, na uoto wa asili iliyoharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu. Bodi imekusudia kuadhimisha siku hii ya mazingira kwa kupanda jumla ya miti elfu moja (1000) katika chanzo cha maji cha Iyofyi-Lungemba katika wilaya ya Iringa na chanzo cha Kibena kilichopo Mafinga Mji.
Hivyo napenda kuchukua nafasi hii kuziomba jamii hususani wale waishio maeneo ya vyanzo na wadau wetu wote kwa ujumla kuungana nasi katika kutunza vyanzo vya maji na kuhamasisha utunzaji wa misitu na uoto wa asili ili kuendelea kuchangia katika wingi wa mtiririko wa maji katika vyanzo kwa manufaa yao binafsi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.